Na. Ezekiel Mtonyole, Chamwino
Serikali imeshauriwa kuwapa mfunzo ya mara kwa mara maafisa ugani ili kuwajengea uwezo wa kuwafundisha na kuwasaidia wakulima namna bora ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazotokana na mabadiliko ya mifumo ya kilimo hapa nchini.
Wakizungumza wakati wa maonyesho maalumu ya mbegu na vyakula asilia yaliyofanyika Wilayani Chamwino, Mkoani Dodoma, baadhi ya wakulima wadogo wadogo walisema changamoto hizo ni pamoja na mabadiliko ya tabia nchi, matumizi bora ya mbegu, mbolea pamoja na janga la uchakavu wa udongo.
Akiongea kwa niaba ya wakulima hao Mwenyekiti wa Jukwaa la Wakulima wadogo wilayani Chamwino (JUWACHA) Mkoani Dodoma chini ya ufadhi wa Shrika lisilo la Kiserikali Action Aid Janeth Nyamayahasi amesema Maofisa Ugani wanashindwa kutoa elimu ya kutosha pamoja na matumizi bora ya ardhi na mbegu bora kutokana na ukosefu wa mafunzo ya mara kwa mara.
"Kuna haja ya serikali kuona namna ya kuwapa elimu wataalamu wa kilimo, hasa kipindi hiki mabadiliko ya tabia ya nchi na kuwajengea uwezo wakulima namna ya kukabiliana na changamoto hiyo" amesema Janeth.
Akiendelea kufafanua amesema maofisa ugani wengi wanashindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa madai yakukwamishwa madaraka kama maafisa ardhi.
Hata hivyo amesema miongoni mwa Changamoto zinazowakabili wakulima ni pamoja na uhaba wa pembejeo na zikipatikana zinachelewa kufika kwa wakati, ukosefu wa masoko ya uhakika na uhaba pia wa maofisa ugani.
Licha ya hayo yote, amelipongeza Shirika la Action Aid kwa kuwa mstari wa mbele katika jitihada za kuwawezesha wakulima wanawake wadogowadogo vijijini kulima kwa kufuata kanuni za kitaalamu na kuwajendea uwezo wa kuweza kumiliki ardhi.
Kwa upande wake, Mratibu wa Shirika la PELUM Tanzania, Donati Senzia, amesema lengo la maonyesho hayo ni kuhamasisha jamii juu ya matumizi ya chakula cha asili,kuhamasisha jamii kuendeleza mfumo wa mbegu za asili na kuwakutanisha wakulima na wataalamu wa mbegu.
Taasisi na mashirika mengine yaliyoshiriki katika maonesho hayo ni pamoja na Wakala wa Mbegu Tanzania (ASA), Kituo cha Tafiti za Kilimo Tanzania (TARI), AGRA na RIPAT.

Comments
Post a Comment
Yes