Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC), Profesa Lazaro Busagala amewataka watumishi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kuhakikisha wanafanyia kazi mafunzo waliyoyapata ya ukaguzi wa mizigo kwa njia ya teknolojia ya Nyuklia kwa lengo la kuongeza ufanisi bandarini hapo.
Mafunzo hayo ya wiki mbili ya ukaguzi wa mizigo kwa kutumia teknolojia ya Nyuklia yametolewa kwa wafanyakazi 22 wa Kitengo cha Midaki (scanner) katika Bandari ya Dar es Salaam ambapo yamelenga kuwapa uwezo wafanyakazi wanaoshugulikia ukaguzi wa mizigo katika midaki (Scanner) katika eneo la Bandari kwa lengo kuongeza kasi na weledi katika ufanyaji kazi kwa lengo la kuharakisha ukaguzi wa mizigo Bandarini.
“Hakikisheni mnatumia mafunzo haya katika kufanya kazi kwa weledi na kuongeza tija ili kusiwe na ucheleweshwaji wa mizigo hapa bandarini,” amesema Profesa Busagala.
Pamoja na mambo mengine, Profesa Busagala amesema TAEC itaendelea na jukumu lake la kutoa mafunzo ili kuhakikisha usalama katika maeneo yote yenye vyanzo vya mionzi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Midaki (Sscanner) Bandarini, Mtani Rugina amesema wataendelea kuhakikisha wafanyakazi wote waliopo kwenye maeneo ya ukaguzi wa mizigo bandarini hapo wanapata mafunzo ili kuboresha ufanisi katika ufanyaji kazi wao.
Comments
Post a Comment
Yes